Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake – 2 | Swahili | Al-Iman Official
Al-Iman Society of Northamptonshire

Society of Northamptonshire, Based in Northampton Mosque and Islamic Centre, 72 Clare St, NN1 3JA

Email: info@al-iman.co.uk

Phone: 07961 284919

Registered Charity: 1117020

© 2018 by Al-Iman - All materials are Copyrights to Al-iman  |  Terms of Use  |   Privacy Policy

Aug 4, 2018

Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake – 2

0 comments

Imekusanywa Na: Abu Faatwimah Makatazo yaliyothibiti maalumu kwa waumini wa kike ni kama yafuatayo: Katazo La Kuunganisha Nywele Tendo hili kwa huzuni kubwa limekuwa ni katika yenye kuonekana kuwa ni miongoni mwa mapambo, bali ni pambo lisiloepukika kwa kila mwenye kutaka kujiremba hasa kwa wenye kutaka kuolewa; wawe hawana nywele au wenye nywele ngumu/fupi au hata wenye nywele za singa; yote kutaka kuiga na kujifananisha na kudanganya, kwa kuwa tuko mbali na yaliyopokelewa kutoka kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kuunganisha nywele.

Kutoka kwa Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema: Alikuja mwanamke kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:"Ee Mjumbe wa Allaah! Hakika mimi nina binti ambae ni bibi harusi, amepatwa na maradhi –surua- hivyo nywele zake zimenyonyoka; je, niziunganishe?" Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Allaah Amemlaani mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwanamke mwenye kutaka kuunganishwa nywele" [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa mwenye kuunganishwa nywele, Hadiyth namba5515].
Na kutoka kwa bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kuwa palikuwa na mjakazi aliyeolewa miongoni mwa wanawake wa ki-Answaar, na huyo mjakazi alipatwa na maradhi yaliyopelekea kunyonyoka nywele zake, basi watu wake wakataka kuziunganisha nywele zake, wakamuuliza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na kuunganisha nywele? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:"Amelaaniwa mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwanamke mwenye kutaka kuunganishwa nywele". [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa kuunganisha katika nywele, Hadiyth namba 5508 na 5509 na 5510].

Kwa hakika hichi kitendo cha kuunganisha nywele si miongoni mwa matendo yanayostahiki kutendwa na wenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah; kwani ni katika matendo na mitindo yenye kufanya na wasioamini Allaah na Siku ya Mwisho –wake kwa waume-, na hili liko dhahiri katika ulimwengu wetu; hivyo kwa mwanamke mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kuunganisha nywele au kutaka kuunganishwa huwa anajifananisha na makafiri, na hilo limekatazwa kama ilivyopokewa kuwa Sa’iyd bin Musayyib amesema kuwa: “Alikuja Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) Madiynah mara ya mwisho aliyokuja Madiynah akatuhutubia, basi akatoa donge la nywele [za bandia] akasema: Sikuwahi kumuona mtu yeyote anafanya haya isipokuwa Mayahudi; kwa hakika Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekiita kitendo hichi Az-Zuura: yaani mwenye kuunganisha nywele” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa kuunganisha katika nywele, hadiyth namba 5512; na Muslim, katika Kitabu cha Mavazi na Mapambo, mlango uharamu wa kitendo cha mwenye kuunganisha nywele na mwenye kutaka kuunganishwa, Hadiyth namba 3976]. Hadiyth hizi ziko wazi kabisa katika kuharamishwa kuunganisha nywele kama alivyosema al-Imaam An-Nawawiy na kulaaniwa kwa muunganishaji na mwenye kutaka kuunganishwa. Tendo hili -la kuunganisha nywele- ni katika madhambi makubwa kwa kumthibitikia Laana ya Allaah mwenye kufanya au kufanyiwa tendo hili; lakini kwa masikitiko makubwa kabisa juu ya kuthibiti Laana ya Allaah kwa watu hao [muunganishaji na mwenye kutaka kuunganishwa nywele] bado kuna wanawake wengi kabisa wenye kufanya tendo hili la kuunganisha nywele za wanawake wenzao au wenye kutafuta wa kuwaunganisha nywele kwa kisingizio cha kujiremba na kujipamba huku wakidai kuwa wao pia ni miongoni mwa wenye kumfuata na kumpenda Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni vyema ieleweke kuwa mwanamke akijipamba ikiwa si kwa ajili ya mumewe basi huwa haramu; na ikiwa atajipamba kwa ajili ya mumewe haitakiwi kujipamba au kujiremba isipokuwa kwa kilichohalalishwa na kukubaliwa na Shariy’ah ya Allaah; kwani haijuzu kwa mwanamke kujipamba kwa ajili ya mumewe kwa kitu Alichoharamisha au Alichokikataza Allaah. Katazo La Kujichora [Tattoo], Kunyoa Nyusi Na Kuchonga Meno Matendo haya matatu yote yamekatazwa; kwa kuthibiti laana kwa mwenye kuyafanya kwa kuwa ndani yake kuna kubadilisha maumbile ya Allaah. Matendo haya pia ni katika yenye kuonekana kuwa ni miongoni mwa mapambo na ni mtu kujitengeneza kwa namna atakavyo, kwa kuwa Muumba –wal –‘iyyaadhu bilLaahi- hakuwa na ufanisi wa kuwaweka vile watakavyo wenyewe katika kuwaremba kwa rangi na chapa tofauti iwe kwa mapicha zikiwemo za wanyama na kadhalika; huku wakisahau kuwa Muumba amesema:

“Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa” [At-Tiyn 95: 4].

Mambo haya kwa baadhi ya ndugu zetu hasa waliobahatika kupata fursa ya kukutana au kuwaona makafiri yamekuwa ni uthibitisho wao wa kuwathibitishia wengine kuwa wao waliwahi kufika Ulaya na katika waliyoyaona ni huku kujichora, kujipiga chapa na kadhalika. Msiba huu wa kujiremba na kujichapa kwa kijichora umewasibu pia baadhi ya waliojaaliwa kuwa wanaume, yote kwa kuwa hawana shukurani kwa kuumbwa waume wala hawaelewi thamani yake; hivyo kwa kupenda kuiga na kujifananisha mtu hujisahau mpaka akafikia kutojikumbuka kuwa umbile lake lilikuwa namna ipi.

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema kuwa: Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwanamke mwenye kutaka kuunganishwa nywele, na mwanamke mchanjaji [mwenye kuwachanja wanawake wenzake kwenye sehemu yoyote ile ya mwili] na mwanamke mwenye kutaka kuchanjwa.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa mwenye kutaka kuchanjwa, Hadiyth namba 5511, 5514,5516 na 5521].

Ama kunyoa au kunyolewa nyusi ni janga jengine; kwani imekuwa ni katika mapambo kwa kila mwenye kutaka kujiremba hasa kwa wenye kutaka kuolewa. Na kutokana na 'AbdullAah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba: “Allaah Amewalaani wanawake wenye kuwachanja wenzao [tattoo], na wanawake wenye kuchanjwa, na wanawake wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wanawake wenye kunyolewa nyusi; na wanawake wenye kuchonga meno kwa urembo [kutengeneza mwanya wapate kuonekana kama ni wasichana, kwa kuwa mwanya hupendeza kwa wasichana] kwa ajili ya kujipamba; wanawake wenye kubadilisha maumbile ya Allaah”; akasema: Hadiyth hii ikamfikia mwanamke kutoka Bani Asad aliyekuwa akiitwa kwa jina la Ummu Ya’quub, mwanamke huyu alikuwa msomaji wa Qur-aan, aliposikia Hadiyth hii alikuja kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) na kumwambia kuwa: “Kilichonileta kwako ni Hadiyth niliyofikishiwa kuwa wewe umewalaaani wanawakewenye kuwachanja wenzao na wanawake wenye kuchanjwa; na wanawake wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wanawake wenye kunyolewa nyusi; na wanawake wenye kuchonga meno kwa ajili ya urembo; na wanawake wenye kubadilisha maumbile ya Allaah”; yule mwanamke akamuuliza kuhusu jambo hili? Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akamwambia:"Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na aliyelaaniwa katika Kitabu cha Allaah!. Yule mwanamke akasema: “Kwa hakika nimesoma baina ya magamba mawili ya msahafu [Kitabu cha Allaah chote kwa ukamilifu] mbona sijakutana na hilo?!” Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akamwambia: “Kama ulikisoma kwa ukamilifu basi bila ya shaka yoyote ile ulikutana na hilo; Allaah Aliyetukuka Amesema:“Na anachokupeni Mjumbe chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho” [Al Hash-r 59:7]. Yule mwanamke akasema: “Hakika mimi naona kuna jambo kama hili kwa mkeo hivi sasa; Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akamwambia: “Nenda ukaangalie vyema”, Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema: “Yule mwanamke aliingia ndani kwa mke wa 'Abdullah lakini hakuona kitu alichodai kuwa anacho huyo mke wa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu)”; yule mwanamke akasema: “Sikuona kitu”; Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema: “Na kama angekuwa anacho hicho ulichodai kuwa anacho basi nisingelimuingilia” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suuratul Hashr, Hadiyth namba 4534; na katika kitabu cha al-Libaas, mlango wa mwanamke mwenye kutaka kuchanjwa, Hadiyth namba 5522; na mlango wa wanawake wenye kunyoa nyusi, Hadiyth namba 5506, 5513 na 5517; na Muslim, katika Kitabu cha Mavazi na Mapambo, mlango uharamu wa kitendo cha mwenye kuunganisha nywele na mwenye kutaka kuunganishwa, Hadiyth namba 3973].

Na kutoka kwa Abu Juhayfah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: “Amekataza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) [Kutumia] thamani ya damu, thamani ya mbwa, pato la mhasharati; na amemlaani mwanamke mwenye kuwachanja wenzake na mwanamke mwenye kutaka kuchanjwa; na mla ribaa na wakala wake; na mchora picha”

[Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na jaza ya Swayd [kuwinda], Hadiyth namba 2095; na katika kitabu cha Al-Libaas, mlango wa mwenye kuchanja, Hadiyth namba 5519.; na katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 5535]. Matendo haya yote –kujipiga chapa, kunyoa nyusi na kuchonga meno- ni haramu kwa mtendaji na mwenye kutaka kutendewa kutokana na Hadiyth hizo, na pia matendo hayo yote ni katika yenye kueleweka kuwa ni kubadilisha maumbile ya Allaah, na ni udanganyifu. Kuthibiti Laana ya Allaah kwa mwenye kufanya au kufanyiwa matendo haya inathibitisha kuwa matendo hayo ni katika madhambi makubwa pia, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa bado kuna wanawake tena wengi sana wenye kutaka kuolewa hufanya matendo haya au hufanyiwa; ili wadhaniwe kuwa ni wasichana wadogo au wadhaniwe kuwa ni wenye nyuso nzuri na za kuvutia; la kusikitisha na kuhuzunisha zaidi ni kule kwa baadhi ya kina mama kuwapeleka wasichana wao wadogo kufanyiwa matendo haya. Huenda likazuka suala hapa; je wale wanawake wenye kuota ndevu au masharubu inaruhusiwa kwao kuzinyoa au kuyanyoa? Jawabu: Naam, inajuzu kwa wanawake kama hawa kuzinyoa ndevu zenye kuota katika nyuso zao au masharubu; na wala hawaingii katika laana; bali kwa kuzinyoa hizo ndevu na hayo masharubu watakuwa wanatekeleza agizo la Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuwataka wanawake wasijifananishe na wanaume, na kwa wanawake kama hawa hawana njia ya kutojifananisha na wanaume isipokuwa kunyoa hizo ndevu au hayo masharubu; na watakapoziacha hizo ndevu au hayo masharubu watakuwa wamejifananisha na wanaume na huko ndiko kwenda kinyume na agizo la Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Pia ikiwa mwanamke atahitaji kuchonga meno yake kwa sababu za kimatibabu au kuondosha aibu katika meno; mwanamke huyu haingii katika laana wala kufanya hivyo haitokuwa haramu kwake kwa kuwa neno

“...kuchonga meno kwa urembo”

lililotumika katika Hadiyth linaonyesha wazi kuwa uharamu uko kwa mwenye kuchonga kwa ajili ya kutafuta urembo na uzuri, hivyo wakati wowote ule atapohitajia mwanamke kuchonga meno yake kwa ajili ya kimatibabu huwa hana dhambi, Allaahu A‘alam. Katazo La Kutoka Nje Huku Akiwa Amejitia [Ananukia] Manukato Moja katika madai ya wanawake ni kuwa mtu si vizuri kusikiwa harufu mbaya [majasho]; juu ya kuwa kuna waume ambao hawasikia harufu nzuri za wake zao isipokuwa pale wanapotoka kwenda katika maharusi; katika kulidhibiti hilo huwa wanapotoka kwa kutaka kutimiza mahitajio yao, kwenda shughulini au shughuli zao za kawaida hujitia manukato yenye kuhanikiza, udi, mafuta mazuri, mafuta ya nywele yenye kunukia au mafuta ya kujipaka mwilini yenye kunukia au hata wanapokoga hutumia sabuni zenye kunukia ili wawe na harufu wanapotoka; desturi hii inawapeleka wengine kushikamana nayo hata wanaposaidiwa kupelekwa pahala kwa gari iwe ya kulipa au ya rafiki wa mume [akiwa na huyo mume mwenyewe ndani ya gari] au hata kwenda Misikitini hujimwagia manukato na kusikiwa na kila mtu awe mpita njia, dereva, na kadhalika. Kwa anayeelewa basi huu ni msiba, na msiba huwa mkubwa zaidi kwa asiyeelewa; kwani jamii yaonyesha kuwa si kuwa iko mbali tu na mafundisho aliyokuja nayo Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali jamii imeyatupa mbali na kuyadharau mafundisho na kila lenye kuambatana na mafundisho hayo. Kutoka kwa bibi Zaynab ath-Thaqafiyyah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

"Atakapo shuhudia mwanamke mmoja wenu Swalah ya 'Ishaa [na katika riwaayah: Msikitini] basi asiguse manukato usiku huo” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah, mlango wa kutoka wanawake kwenda Misikitini ikiwa haitosababisha fitnah na hali yeye..., Hadiyth namba 678 na namba 679].

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

”Mwanamke yeyote yule ataejifukiza udi [harufu nzuri] basi asishudie pamoja nasi Swalah ya ‘Ishaa ya mwisho” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah, mlango wa kutoka wanawake kwenda Misikitini ikiwa..., Hadiyth namba 680.]

Na kutoka kwa Abu Muusa Al-Ash-‘ariy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

”Mwanamke yeyote yule ataejitia manukato akapita mbele ya watu ili waipate harufu yake basi huyo ni mzinifu [atakuwa amezini]” [Imepokelewa na Ahmad katika musnad wake, kitabu Musnad wa watu kumi waliobashiriwa pepo, hadiyth ya Abi Musa Al-Ash-‘ariy (Radhiya Allaahu 'anhu), Hadiyth namba 19272 na 19305; na at-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Adabu, mlango wa yaliyokuja katika yenye kuchukiza kutoka kwa mwanamke ..., Hadiyth namba 2730].

Hadiyth hizi zote dada yangu katika iymaan zinathibitisha uharamu wa kutoka nyumbani kwako hali ya kuwa unanukia, kwani manukato au harufu yake haraka huwafanya wanaume wavutiwe na kupata matamanio ya kutaka kumkaribia aliyejipaka hayo manukato. Katika kusherehesha neno [huyo ni mzinifu] Wanazuoni wanasema kuwa

“Amezini kwa kuwa amesababisha kuzindua matamanio ya wanaume kwa hiyo harufu wanayoipata inayotokana na manukato [au udi] aliyojitia; jambo linalowapelekea kutaka kuelewa nani huyo mwenye kunukia na hilo huwapelekea kumkodolea macho; na mwenye kumtazama huwa amezini [zinaa ya macho], kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ameandikiwa kila mwanaadamu sehemu yake katika zinaa; hakuna njia ya kuiepuka; macho mawili zinaa yake ni kutazama, masikio mawili zinaa yake ni kusikiliza, na ulimi zinaa yake ni kusema, na mkono zinaa yake ni kuunyoosha, na mguu zinaa yake ni hatua zake, na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha au kukadhibisha” [Imepokelewa Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 6152; na Muslim, katika Kitabu cha Qadar, mlango wa imekadiriwa juu ya kila mwanaadam sehemu yake katika zinaa, Hadiyth namba 4808 na namba 4809].

Ni jambo linaloeleweka kuwa kumtazama mwanamke ni katika vitangulizi vya zinaa ya sehemu za siri za wanaume, hivyo ni wajibu kwa kila dada mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kutotoka nyumbani kwake isipokuwa kwa haja [dharura] yenye kukubalika na Shariy’ah, na hapo atapohitaji kutoka, basi ahakikishe kuwa anajipamba kwa adabu za kishariy’ah ambazo miongoni mwake ni kuwa amejifunika na kujisitiri vizuri kwa hijabu ya kishariy’ah; na wakati wowote ule ataporudi nyumbani kwake yuko huru kujitia manukato atakavo, kwa sharti kuwa hawatoipata harufu ya manukato yake wanaume wengine wasio kuwa maharimu zake. Katazo La Kudhihirisha Mapambo Kwa Wanaume Allaah Aliyetukuka Anasema:

“Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijaahiliyyah...…” [Al-Ahzaab 33: 33].

Amesema Mujaahid:

“Walikuwa wanawake wanapotoka nje ya nyumba zao hujipitisha mbele za wanaume, na huko ndiko kujishauwa kwa majishauwo ya kijaahiliyyah.”

Amesema Qataadah:

“Walikuwa wanawake wanapotoka nje ya nyumba zao, hutembea ovyo pasina hayaa na huku wakijitikisa tikisa, na ndio Allaah Aliyetukuka Akawakataza.”

Amesema Muqaatil bin Hayyaan:

“Tabarruj ni pale mwanamke anapokuwa ameweka Khimaar [shungi] kwenye kichwa chake lakini akawa hakuifunga itakiwavo, hivyo mkufu [kidani], vipuli [herini], shingo yake na vyote hivyo vikawa vinaonekana”.

Wanawake wanakatazwa kujishauwa na kujitikisa tikisa wakati wakiwa wako nje ya nyumba zao; na huwa ubaya zaidi pale wanapokuwa wamejipamba kwani kutawapelekea wanaume wawatazame na kuyaona mapambo yao; wanawake hawa huwa na mitindo ya kimaajabu ya kupiga viatu vyao chini na kadhalika. Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Aina mbili za watu ni miongoni mwa watu wa Motoni sijawahi kuziona: Watu ambao wana fimbo [mijeledi] kama mikia ya ng'ombe dume ambazo wanawapigia watu, na wanawake ambao wamevaa lakini wako uchi; wanawashawishi wanaume wawatongoze, na wanaelekea kwao [kwa kuwa warahisi]; vichwa vya wanawake hao kama nundu za ngamia zinazoyumba; hawatoingia Peponi na wala hawatoipata [hawatosikia] harufu yake, na harufu yake inaweza kusikiwa kutoka masafa kadhaa na kadhaa” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Jannah na sifa za na’iyma zake na watu wake, mlango wa Moto watauingia majabari na Pepo wataiingia madhaifu, Hadiyth namba 5103; na katika Kitabu cha Mavazi na mapambo, mlango wa wanawake Al-Kaasiyaat Al’Ariyaat Al Maailaati.., Hadiyth namba 3978].

Angalia dada yangu katika iymaan makemeo makali hayo na mazito na adhabu inayomsubiri mwenye kujifakharisha kwa uzuri wake na kudhihirisha mapambo yake kwa wanaume wasio kuwa maharimu zake; huenda kwa mwanamke kudhihirisha mapambo yake kwa wanaume hapa duniani ikawa furaha, fakhari, pato zuri [kama wenye kushiriki katika mashindano ya mwanamke mzuri] tija na umaarufu; lakini itakuwa hasara na majuto Siku ya Qiyaamah, kwani itakuwa ni sababu tosha kwa yeye kujiharamishia Jannah na kutumbukizwa Motoni. Ewe mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah! Jihadhari na kudhihirisha mapambo yako kwa wanaume wasiokuwa maharimu zako; jihadhari sana na kutojisitiri vizuri kwa hijabu ya kishariy’ah utokapo nje ya nyumba yako, au hata ndani ya nyumba yako wakiwepo wasiokuwa maharimu zako; jihadhari na kujitia manukato, udi na mfano wa hivyo wakati unapotoka nje ya nyumba yako; jihadhari na kupatikana harufu ya manukato yako na wanaume wasiokuwa maharimu zako; yote hayo dada yangu katika iymaan ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako na ni katika yenye kukupelekea kuwa miongoni mwa wenye kuwajibikiwa adhabu Siku ya Qiyaamah.

New Posts
  • KUNUIA HAJJ NA UMRA Labbayka Allahumma Umra Nimekuitikia Ewe Mola, (nimenuilia) Umra Labbayka Allahumma Hajj Nimekuitikia Ewe Mola, (nimenuilia) Hajj TALBIYAH Labbayka-Llaahumma labbayk labbayka laa shariyka laka labbayk inna-l hamda wa-n ni'mata laka wa-l mulk, laa shariyka lak Tumeitikia Ewe Mola tumeitikia, Tumeitikia kwani huna Mshirika Tumeitikia, Hakika Himdi (shukurani) na Neema zote ni zako na Ufalme ni wako na huna mshirika. KUINGIA MSIKITINI Allaahumma salli `alaa muhammadin wa sallim, allaahumma aftah lee abwaaba rahmatika. Allah, Msalie muhammad na umfikishie salamu, O Allah nifungulie milango ya rehma zako.. KATI YA KONA YA YAMANI NA JIWE JEUSI Rabbanaa aatinaa fi-d dunyaa hasanatan wa fi-l aakhirati hasanatan wa qinaa 'adhaaba-n naar. Allah tunakuomba utupe yenye kheri katika dunia na yenye kheri akhera na utuepushe na adhabu ya moto. KUNYWA MAJI YA ZAMZAM Ibni Abdallah ibn Abbas alikuwa akiomba kwa kusema Allahumma inni as’aluka I’lman naafian wa rizkan waasian wa shifa’an min kulli daain O’ Allah ninakuomba elimu yenye manufaa na riziki yenye kujitosheleza na shifaa kutokana na kila maradhi. SAFA NA MARWA Inna-s safaa wa-l marwata min sha'aa'iri-l llaahi faman hajja-l baita aw i`tamara falaa junaaha 'alaihi an yattawwafa bihimaa wa man tatawwa'a khairan fa inna-l llaaha shaakirun 'aleem. Hakika vilima vya Safa na Marwa ni katika alama za Allaah. Basi anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anayejitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Allaah ni Mwenye shukrani na Mjuzi.” ARAFAT "Laa ilaha illallaahu wahdahu laa shareeka lahu lahul mulk wa lahul hamdu wa huwa 'alaa kulli shay'in qadeer.” Hakuna Mola anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah pekee, hana mshirika, Ufalme wote ni wakeZ na himidi ( shukurani) zote ni kwake naye ni muweza wa kila jambo.
  • Ummu Nasra  Kuna mambo mengi ya wazi kabisa ambayo sheria yameyakataza katika Uislamu na jamii imeghafilika nayo.  Mambo hayo huchangia  kuharibika na kuhatarisha mfumo  mzima wa kiislam ndani ya majumba. Miongoni mwa yenye kuhatarisha ni haya yafuatayo: 1. TELEVISHENI (TV) - LUNINGA. Televisheni kama inavyojuilikana (TV) ni chombo ambacho hakikosekani katika kila nyumba.  Kama kitatumika vizuri chombo hicho kwa mambo ya kheri yenye kuzidisha imani, kupeleka dini mbele, kukuweka mbali na maasi na kuhifadhi dini ya mja kinaweza kuleta faida.  Na kama kitatumika vibaya kinaweza kuathiri familia kwa asilimia kubwa kabisa.Ukweli ni kuwa kuangalia TV kuna madhara mengi na makubwa kuliko faida. Familia za kiislam zinaogelea kwa kasi kubwa bila ya kujali au kuona mabaya ya chombo hicho. Tuchukue mfano mdogo tu wa athari za televisheni kwa watoto kama utafiti huu mdogo uliofanyika hapa Uingereza unavyofafanua. Watoto wenye kuangalia televisheni kwa zaidi ya masaa mawili kila siku wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa athma. Uchunguzi huo umeonyesha kuwa, kuangalia televisheni kwa muda mrefu kunaleta uwezekano wa kupata athma uongezeke mara mbili kwa watoto. Jinsi mfumo wa kupumua unavyofanya kazi wakati mtoto anapokaa tu bila kufanya chochote, hupelekea kutokea mabadiliko katika mapafu pamoja na magojwa mengine ya kupumua ikiwemo athma. Unene wa kupita kiasi pamoja na kutokufanya mazoezi kunakosababishwa na kuangalia muda mrefu televisheni hupelekwa kutokea hali hiyo Wataalamu wamesema kuwa, kuishi maisha ya kutokuwa na harakati yoyote katika umri mdogo hupelekea kuongezeka uwezekano wa hatari ya kupata athma ukubwani.Hivyo wamewashauri wazazi kuwashajiisha watoto wao kufuata maisha ya kawaida ya kuwa na mishughuliko na kupunguza muda wanaoutumia kuangalia TV. Wataalamu wa Uingereza wametoa taarifa hiyo baada ya kuwafanyia uchunguzi watoto 3,000  kuanzia wale waliozaliwa mpaka walio na miaka 11. Hasara moja ya kupoteza muda kuangalia TV inaweza kuzaa makosa mengi ndani yake.  Kuona na kusikiliza kuna wavutia wengi na kuwafanya watu kutawaliwa na tabia hiyo na kutoweza kuiepuka. Hakuna shaka kuwa jamii hasa watoto imeathirika sana na jambo hili.  TV inasababisha kwa kiasi kikubwa watoto wa Kiislamu kutumbukia katika tabia zisizo na maadili, ulevi, uzinzi, kukosa heshima, kujinasibisha na uzungu na mengi mengine maovu tunayoyaona katika jamii zetu.  Yote hayo wanayaona na kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye TV.Mtu huhisi kuwa anapoteza wakati tu kujistarehesha na TV, anayakata masaa na dakika kwa ajili ya chombo hicho, ni makosa!!.   TV si chombo cha starehe, bali ni chombo kinachotumika kuchochea hisia, kubadilisha muelekeo na utiifu wa mtu. Na ndiyo hali halisi ndugu yangu Muislamu kama bado hujatanabahi.Yafaa Waislamu tuzinduke na kuziona faida chache na hasara nyingi za chombo hiki.  Kama tunaona ni neema hakika tutakuja kuulizwa namna tulivyoitumia.  [At-Takaathur 102:8] ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ - 102:8 Kisha mtaulizwa siku hiyo juu ya neema mlizopewa mlizitumiaje. Na kwa hakika hata  masikio na macho tunayoyatumia kwa chombo hicho pia tutakuwa ni wenye kuulizwa. Hivyo ni juu yetu kuchagua ni kipi cha kutizama. [Al-Israa 17:36].  وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا - 17:36 Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa Tv ni kama upanga ukiutumia vizuri unaweza kuleta faida na ukiitumia vibaya unaweza kuleta madhara makubwa.  Kwa mfano mtu akiweza kuidhibiti na kuangalia kwa nadra kwa vipindi vya kheri vyenye kwenda sambamba na dini yetu inaweza kukubalika, bali ni wachache wenye kufanya hivyo.  Wengi wao wameogolea na kuangalia tu bila hata ya kujali faida na hasara zake, na hii ndio iliopelekea madhara kuwa mengi kuliko faida.  Miongoni mwa madhara ya TV ni:- Kunapoteza wakati bure na kupuuza mengi ya wajibu- Inaeneza tamaduni za kikafiri kama ni njia moja ya kuigwa katika maisha- Inaeneza upotofu na uhuru kwa kupitia katika michezo, nyimbo matangazo yasiyo ya heshima ambayo hupelekea watizamaji kutumbuka na tabia hizo za kijinga.- Mazoea ya kuangalia TV yanaharibu akili na kuathiri afya ya mja. Hivyo kama kuna watu wazuri wenye kumuogopa Allah  Subhaanahu Wata’ala na kuonyesha mazuri yenye faida bila ya kukiuka mipaka ya Allah, basi unaweza kuangalia na ni jambo la kupendeza kwa wengi. Ni vyema kuchunga aina gani ya vipindi tunavyoangalia ndani ya majumba yetu.Ni wajibu wa kila mtu kueleweka wazi madhara na faida ya kifaa hichi ili tuweze kukitumia vyema ama kujiepusha nacho kabisa ikiwa tutashindwa kuweka vidhibiti katika majumba jinsi chombo hiki kitumike katika kunufaisha, kuelimisha na kuleta faida na si kuharibu, kupoteza muda na kupelekea jamii iliyozugika na hatimaye kupotoka na kupotosha wengine. Inaendelea IshaAllah.
  • Ummu Nasra  UTANGULIZIHakika shukrani zote ni zake Allaah Subhaanahu Wata’ala, tunaemshukuru, tunaemtegemea, kumtaka msamaha na kutubu kwake. Tunajikinga Kwake Allaah Subhaanahu Wata’ala kutokana na shari za nafsi zetu na makosa ya matendo yake. Mwenye kuongolewa na Allaah hakuna wa kumpotoa, na mwenye kumpotoa hakuna wa kumuongoa. Rehma na Amani ziwe juu ya kipenzi chetu Muhammad SwallaAllahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam.‘Amma Ba’ad Nyumba ni neema kubwa ambayo mwanadamu amebarikiwa, وَاللَّهُ جَعَلَ لَكُم مِّن بُيُوتِكُمْ سَكَنًا وَجَعَلَ لَكُم مِّن جُلُودِ الْأَنْعَامِ بُيُوتًا تَسْتَخِفُّونَهَا يَوْمَ ظَعْنِكُمْ وَيَوْمَ إِقَامَتِكُمْ ۙ وَمِنْ أَصْوَافِهَا وَأَوْبَارِهَا وَأَشْعَارِهَا أَثَاثًا وَمَتَاعًا إِلَىٰ حِينٍ - 16:80 Na MwenyeziMungu amekujaalieni majumba yenu yawe maakaazi (yenu) [An-Nahl 16:80] Kuweka mazingira sahihi ndani ya majumba ni jukumu la kila muislam mume na mke, na ni lazima mazingira hayo yaoane sambamba na sheria alizotuwekea Allah Subhanahu wa Ta’ala. Moja kati ya njia ya kuyafikia hayo ni kuepukana na kila aina ya uovu na uharibifu ndani ya majumba. Kuna sababu nyingi kwa mwenye kuamini kuwa makini katika kuijenga na kuilinda nyumba yake katika misingi mema ya kiislam. Miongoni mwa sababu hizo ni: 1. Kujilinda yeye pamoja na familia yake kutokana na moto wa jahannam, na kujiweka mbali na ghadhabu zake. [At-Tahriym 66:6] يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ - 66:6 Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu na moto ambao ambao kuni zake ni watu na mawe 2. Kujua wajibu wake juu ya jukumu la kuchunga nyumba, na kujiweka tayari kujibu kwa kila unachokichunga. Hadith: Kutoka kwa Abdullah, Allah amuwie radhi, kwamba Mtume SwallaAllahu ‘Alayhu wa Aalihi wa Ssallamamesema: “Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa juu ya mlivyovichunga. Kiongozi anaewaongoza watu ni mchunga na ataulizwa juu wachungwa wake. Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya wachungwa wake. Na mwanamke ni mchunga kwa nyumba ya mumewe na watoto wake nae ataulizwa juu ya wachungwa wake .Mtumwa ni mchunga katika mali ya bwana wake na anawajibika juu ya mali hiyo. Hakika nyote ni wachunga na na kila mmoja wenu anawajibika juu ya wachungwa wake” Imesimuliwa na Bukhari na Muslim 3. Nyumba ni sehemu ya hifadhi kwa binaadamu, kujiweka mbali na kila aina ya ubaya na uovu ukiwa wa mnyama, binaadamu au majini, na kupata utulivu ndani yake. Amesema Mtume SwallaAllahu ‘Alayhu wa Ssallam: Usalama wa mtu katika wakati wa fitnah ni kubakia nyumbani kwake. Kilicho muhimu zaidi ni kuzingatia kuwa nyumba ni sehemu nyeti (muhimu) ya kujenga mazingira mazuri ya kiislam, kwani jamii bora hujengeka kuanzia nyumbani. Kwa masikitiko makubwa majumba yetu mengi yamejiweka mbali na mafundisho sahihi ya kiislam. InshaAllaah katika makala hizi tutaweza kugusia na kutanabahisha baadhi ya vitu ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibika mfumo wa kiislam ndani ya majumba na jamii kwa ujumla, na kujaribu kutafuta njia muafaka kurejesha mazingira mazuri ndani ya majumba yetu. WabiLlaahi Attawfiyq InshaAllah itaendelea..