
UTAMBULISHO
Karibu katika tovuti ya Jumuiya ya Al–Iman ya Northamptonshire. Ni jumuiya ya khiari iliyosajiliwa kwa ajili kusaidia jamii ya kiislamu Northamptonshire - Uingereza Jumuiya imeasisiwa na Waislamu wanaozungumza lugha ya Kiswahili, wanatoka katika nchi za Mashariki ya Afrika na wakaazi wa jimbo hili
Jumuiya haina uhusiano wa aina yoyote na mambo ya siasa na inajihusisha zaidi kama taasisi ya Daawah pamoja na elimu.
Jumuiya ina lengo la kuihifadhi jamii ya waislamu wanaozungumza Kiswahili wasipoteze urithi wao (dini ya kiislamu) pamoja na utamaduni wao kwa kupitia programu za kielimu na harakati za kijamii. Jumuiya inaamini njia hii itawasaidia kuweza kupata mafanikio katika mazingira wanaoishi hapa ambapo ni mchanganyiko wa tamaduni na jamii tofauti.
Jumuiya haipokei msaada kutoka kwenye kitengo chochote nje na ndani ya Uingereza bali inasaidiwa na waislamu wakaazi wanaozungumza Kiswahili pekee katika kuendesha harakati zake.
Jumuiya ilianzishwa mwaka 2001 na kupata hadhi ya kuwa jumuiya ya hiari (charitable status) Novemba 2006. Tokea kuanzishwa kwake jumuiya iliona haja ya kuwa na taasisi muhimu za kiislamu katika jamii kama Madrasah( chuo) , mfuko wa misiba na kituo cha kuweza kutekeleza programu zake. Jumuiya ina mipango endelevu kwa ajili ya kukitunza kizazi chetu na kuweza kuwaendeleza watoto wetu katika njia na mielekeo sahihi.
Wakaazi waislamu wa jimbo hili ndio waliokusudiwa kunufaika na jumuiya hii kutoka miji kama Northampton, Wellingborough, Corby, Kettering, Daventry na Rushden; Hata hivyo muislamu yoyote anakaribishwa kutoa mawazo, maoni, mbinu na kadhalika kwa ajili ya kuiendeleza jumuiya.
Manhaj ya Jumuiya:
Katiba imeeleza bayana kwamba Jumuiya itaongozwa kwa kufuata Qur’aan na Sunnah sahihi za Mtume wake Salla Allah ‘Alayhi Wasallam katika kuiendeleza dini yetu ya kiislamu. Hivyo:
1 Itafuata Qur’aan kwa ufahamu wa Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam pamoja na maswahaba na wema waliotutangulia.
2 Itajitahidi kufuata Sunnah sahihi na kutilia umuhimu wa kufuata Sunnah ikiwa ni dira ya utendaji wa kazi za Jumuiya
Kuna njia tofauti ambazo unaweza kujumuika na Al – Iman kama
Kujiunga kuwa mwanajumuiya – Kwa wale watakaopendelea kujiunga na kuisaidia jumuiya kwa misaada tofauti
Kujiunga kuwa mdhamini – Kwa wale wanaotaka kuchangia harakati za jumuiya ikiwa ni mara moja wa kwa kila baada ya muda.
Kujiunga kama Mwalimu/mwanafunzi – Kwa wale wenye sifa za kusomesha au kutaka kusoma na kuweza kusaidia Madrasah na kuendesha Darsa za Jumuiya.
Kujiunga kuwa mtoa huduma – Kwa wale wataokuwa tayari kutoa huduma kuisaidia jamii itakapohitajika.
Kujiunga kuwa mchangiaji – Kwa wale watakaojiunga katika mfuko wa misiba kusaidia watakaofikwa na fardhi ya mauti.
Kujiunga kama Mlezi – Kwa wale watakaokuwa tayari kuiangalia Jumuiya na kuhakikisha inafuata vilivyo malengo iliyojiwekea
Jumuiya inatoa huduma zifuatazo kwa sasa:
Mihadhara na mijumuiko ya kielimu
Darsa na masomo
Habari na taarifa
Madrasah
Maziko na misiba
Ushauri kwa ujumla
Ndoa
Programu za Ramadhaan
Michezo kwa watoto
Ushauri kwa wanaotaka kufanya ‘Ibada ya Hajj
Ushauri kwa wanaotaka kutoa Zakaah na Swadaqa
Vifaa kwa ajili ya kufanyia shughuli.
Hata hivyo Jumuiya haina uwezo wala fedha za kusaidia:
Wanafunzi wanaotoka nchi za nje wanaosoma hapa Uingereza.
Wanaotaka kutafutiwa wachumba kwa ajili ya ndoa na pia ndoa zinazofungwa kinyume na taratibu sahihi.
Taasisi za kiislamu zilizopo nje ya Uingereza.
Kusafirisha mwili wa marehemu nyumbani alipotoka kwa ajili ya mazishi.
Jumuiya bado ni changa na inahitaji msaada wa kila mmoja wetu kwa kadri na hali aliyonayo kuweza kufikia malengo yake na kutoa huduma na mipangilio iliyo bora kwa ajili yetu kwa pamoja.