Misingi ya Sheria - Maswaadiru Shari'ah
Misingi ya sheria ni chimbuko la elimu yaani dalili na ushahidi wa jambo unapochukuliwa. Sheria yetu ya kiislamu imejiegemeza katika misingi mikuu mine. Miwili ikiwa ni mikuu na miwili ikiwa ni tegemezi kama ifuatavyo:
QUR’AAN
SUNNAH (HADITHI)
IJMAA
QIYAAS
QUR’AAN - MSINGI MKUU
Ni msingi wa kwanza katika misingi mikuu .
Kitabu chake Allah Subhaanahu Wata’ala alichomteremshia Mtume wake (Salla Llahu ‘Alayhi Wasallam)
SUNNAH(HADITHI) - MSINGI MKUU
Ni msingi wa pili mkuu.
Sunnah - Hadithi katika sheria ni kila aliloliamrisha Mtume (Salla llahu ‘Alayhi Wasallam) au alilolikataza au alilolipendekeza katika kauli na vitendo na iqrari- kitendo cha Mtume(Salla Llahu ‘Alayhi Wasallam) kumuona mtu akitenda jambo na asitoe maelekezo yoyote ya kukemea au kukataza.
IJMA’A - MSINGI TEGEMEZI
Ijma’a ni kongamano na makubaliano ya wanazuoni wa kiislamu baada ya Mtume(Salla llahu ‘Alayhi Wasallam) juu ya jambo au suala ambalo halikuelezwa bayana ndani ya Qur’aan au Sunnah
QIYAAS- MSINGI TEGEMEZI
Qiyaasi ni mizani ya kulipima jambo au suala ambalo halina ufafanuzi ndani ya Qur’aan au Sunnah na jambo au suala lililotajwa, kwa kulingana sababu(Illa)zao.
Imeitwa tegemezi kwa sababu ya kutegemea Quraan na Sunnah katika kulipatia hukumu jambo kwa ujumla .
HUKUMU ZA SHERIA YA KIISLAMU
Faradhi/Wajibu
Manduub/Sunnah
Haramu
Mubah/Halali
Makruuh
FARADHI/WAJIBU
Fardhi au Wajibu ni jambo ambalo kila Mukallaf amelazimishwa na sheria kulitenda na jambo lenye limethibitika katika Quraan au Sunnah kwa dalili isiyo na shaka.
MANDUUB/SUNNAH
Jambo linalotatikana na sheria kulitenda kwa kila Mukallaf lakini bila ya kulazimishwa.
Pia hujulikana kwa majina yafuatayo, Mustahab – jambo linalopendeza, Naafilah, Tattawu’u. Na miongoni mwa mambo ya Sunnah zipo za kawaida na nyengine zilizotiliwa mkazo.
HARAMU
Ni lile jambo lililokatazwa kwa mtazamo wa kisheria na kupata adhabu huko akhera tuendako au hapa hapa duniani kwa mwenye kulitenda.
MUBAAH/HALALI
Jambo lililoruhusiwa kisheria au kupewa khiari muislamu katika kulifanya au kutolifanya bila ya kutahadharishwa nalo au kupata dhambi au thawabu.
Asili ya vitu vyote kwanza huwa Mubaah mpaka ipatikane dalili ya kuthibitisha vyenginevyo. Hakuna thawabu wala dhambi kwa kutenda/kutolitenda isipokuwa tu ikiwa halikufanyika linaweza kupelekea madhara kama mtu kukataa/ kugoma kula ataweza kulazimishwa kwa lengo la kuhifadhi nafsi
MAKRUUH
Jambo ambalo linachukiza - linalolikirihisha- kulitenda kwa mtazamo wa sheria. Hastahiki mtu kupata adhabu ya Mola kwa kulitenda bali akiacha atapata thawabu.
MAQAASIDU SHARI’AH – MAKUSUDIO YA SHERIA
Haya ni mambo ambayo sheria yetu ya kiislamu inatutaka tuyahifadhi na kuhakikisha tunayalinda kwa kuyatekeleza ipasavyo.
1 KUHIFADHI DINI- Kuhakikisha dini yeu inasimama katika ardhi na kuwa tayari kuilinda dini hii kwa ajili ya Allah Subahaanahu Wata’aala
2 KUHIFADHI NAFSI- Kuhakikisha haki ya kimsingi ya kila binadamu ya kuishi inatekelezwa na kuifanya haki hi iendelee katika ardhi kwa kutumia njia za halali (ndoa) katika kuongeza kizazi
3 KUHIFADHI AKILI- Kwa kuhalalisha kila chenye kuihifadhi akili na kuharamisha kila chenye kuleta madhara kwa akili kwani akili ni chimbuko la mambo yote ya kheri na moja katika mambo yanayoangaliwa kwenye kukalifishwa
4 KUHIFADHI KIZAZI- Ili kuweza kujenga jamii iliyo salama na madhubuti katika tabia na maadili na pia kuhakikisha kitakachohalalishwa katika maingiliano ya ndoa kimehalalishwa kwa mujibu wa sheria.
5 KUHIFADHI MALI- Mali ndio msingi wa kipato kwa mja hivyo ni wajibu kuhakikisha inahifadhiwa na kupatikana adhabu kwa walioifisidi
SUNNAH
Kilugha lina maana ya njia au mwenendo . Katika kulitafsiri neno hili na jinsi linavyotumika kisheria itabidi tuliangalie katika hali tofauti na maana zake ili tuweze kupambanua wakati linapotumika linakusudiwa kitu gani.
SUNNAH KWA MTAZAMO WA KIHADITHI
Ni kila kilichopokelewa kutoka kwa Mtume Salla llahu ‘Alayhi Wasallaam katika kauli ,vitendo , iqrari , sifa ya kimaumbile , sifa ya kitabia tokea kabla ya kupewa utume mpaka baada ya kupewa utume.
Na katika maana hii neno sunnah na hadithi ni sawasawa
SUNNAH KWA MTAZAMO WA KISHERIA
Ni kila aliloliamrisha Mtume (Salla llahu ‘Alayhi Wasallam) au alilolikataza au alilolipendekeza katika kauli na vitendo na iqrari- [kitendo cha Mtume(Salla llahu ‘Alayhi Wasallam) kumuona mtu akitenda jambo na asitoe maelekezo yoyote ya kukemea au kukataza] Na jambo hili kutumika kama dalili katika hukumu ya kisheria.
SUNNAH KWA MTAZAMO WA KIFIQH
Ni kila jambo ambalo limethibiti kwa Mtume Salla llahu ‘Alayhi Wasallam lakini halipo katika hukumu ya fardhi wala wajibu.
ISTWILAHI
Maana ya neno kwa mtazamo wa kisheria.Mara nyingi maneno yana asili ya lugha ya kiarabu na hivyo kuwa na maana mbili moja ya kilugha – linavyojulikana neno kilugha na maana nyengine ya kiistwilahi – kisheria. Na maana hii ya kisheria ndio inayohitajika kutumika na kufanyiwa kazi.