Yenye Kuhatarisha Nyumba za Waislamu - 3

Ummu Nasra 

2.  MUZIKI NA NYIMBO

Miongoni mwa yenye kuzoeleka katika majumba yetu ni mziki.  Kwa kweli mziki umeenea kila pembe ya dunia kiasi ambacho unawaumiza Waislamu wengi kimwili na kiakili bila ya kujijua.  Kila mtu amekabiliana na hali ambayo humuingiza kusikiliza muziki ama kwa hiari au kwa lazima.   Kuongezeka umaarufu wa muziki kunahatarisha sana majumba ya Waislamu na hatimae kutumbukia katika balaa hilo  usiku na mchana


Ukweli ni kuwa muziki unaathiri sana mioyo ya Waislamu na kuishughulisha akili kwa mambo ya kipuuzi. Tunatumia muda na pesa nyingi katika kununulia CD za majimbo yasiyo na faida, zana za miziki,  na hata kuwatumbukiza watoto wetu kwa vifaa (toys) mbali mbali vilivyojaa miziki; Tunajitia makosani na kuuporomoa itikadi sahihi ya Muislamu. Kuna dalili tosha katika Quraan na Sunnah zenye kuonyesha uharamu wa muziki. Katika Suurat Luqmaan aya ya 6  Allaah Subhaanahu wa Ta'ala anatueleza:


وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ - 31:6
Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha

Maulamaa pamoja na wafasiri wengi wa Quraan wameeleza kuwa neno ”Lahwal-hadith” katika aya hii inakusudiwa nyimbo na zana za miziki. Mfano  Ibn Mas'uud Radhiya Allahu 'anhu amesema kuhusu Aya hii

"Naapa kwa Allah hii inamaanisha ni nyimbo"

Pia miongoni mwa hadithi zenye kuonyesha  uharamu wa ngoma na kila aina ya muziki ni hadithi mashuhuri ya  Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:


“Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muzi -Bukhari

Ni vyema tuelewe kuwa hakuna chochote alichokikataza Allah Subhaanahu wa Taala isipokuwa kina madhara ndani yake katika ustawi wa jamii.  Jua kuwa miziki tunayoichezesha majumbani yanaweza kuchochea hisia za mja, jazba pamoja na muengezeko wa mapigo ya moyo na kushughulisha akili. 


Ujumbe unaopatikana katika miziki na nyimbo nyingi hasa wakati huu tulionao huenda kinyume kabisa na maadili ya Kiislamu, huamsha hisia za mapenzi, uzinzi na uhuru wa kufanya lolote bila ya kuzingatia wajibu wa mja. 

Umefika wakati kwa Waislamu kutanabahi na kujaribu kwa kadiri ya uwezo wetu kuepukana na balaa hili na kurejesha mandhari nzuri ndani ya majumba yetu.  Tusiziuwe nyumba zetu kwa sauti za shetani (nyimbo na miziki) na kuwawekea makaazi,  Ni lazima tuziuhishe nyumba zetu kuwa ni sehemu ya kumkumbukwa Allah Subhaanahu wa Taala (dhikr) kwa kila hali; kwa sala, kusoma Quraan, na vitabu vyengine vya dini pamoja na  masuala mbali mbali yanayowahusu Waislamu.  Hii itatupelekea kuzungukwa na Malaika, kulindwa na kupata ridhaa ya Allah Subhaanahu wa Taala.MCHANGANYIKO WA WANAUME NA WANAWAKE (IKHTILAATW)

Moja katika jambo linaloonekana ni la kawaida hasa katika majumba yetu ni michanganyiko ya wanaume na wanawake (Ikhtilaatw).  Ni wajibu wa kila Muislamu kuelewa hukumu ya kisheria juu ya jambo hili.

Ikhtilaatw ni kuchanganyika kwa  wanawake na wanaume waliokuwa sio maharim ima kwa wingi au uchache katika sehemu moja. Hali hii imezoeleka sana majumbani mwetu, katika shughuli zetu zikiwa ni za furaha au misiba au hata  siku za kawaida. 

Tuelewe kuwa mijumuiko ya aina hii na kudhihirika mapambo ni kitu kilichokatazwa katika sheria kwa sababu huwa ni mzizi wa fitina na ni kichochezi cha maasia mengine kwani shaytwan huwa pamoja nao.  Katika hadithi iliyosimuliwa na ‘Umar, Radhiya Llahu ‘Anhu inatueleza:

Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao. [At-Tirmidhiy]

Dini yetu imetuwekea adabu maalum; na kama kuna ulazima wa kuchanganyika majumbani,  basi ni vyema kuwe na sehemu tofauti kati ya wanaume na wanawake pindi wakikujia kwao.  Tunatakiwa tuwe na hadhari tunapotembelewa na mgeni, hata kama ni ndugu wa mume au mke. Mtume Swalla Llahu ‘Alayhi wa Ssalaam aliwaeleza maswahaba zake na Waislamu wote kuwa:

Tahadharini kuingilia majumbani mwao wanawake; Wakasema: Ewe Mjumbe wa Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: Shemeji ni mauti- Al-Bukhaariy na Muslim]

Pia Allaah Subhanahu wa Taala anatueleza katika Suuratul Al-Ahzaab:53

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ
Nanyi mnapowauliza (wakeze) waulizeni nyuma ya pazia.  Kufanya hivyo kunasafisha nyoyo zenu za zao.

Ni jukumu letu kama ni wazazi kuzielewa sheria hizi na kuzidi kuzipamba nyumba zetu katika mandhari nzuri ya kiislam.  Hii itasaidia hata na vizazi vyetu kuinukia kwa maadili na tabia njema na kujua mipaka yao. Na kama itatokea kwa mwanamme au mwanamke kutembea au kutembelewa  na kukutana na mwenyeji wa jinsia tofauti basi na tumuogope Allaah na kujihifadhi kwa kadiri ya uwezo wetu, bila ya kurefusha mazungumzo. 

Allaah Alietukuka Anatufahamisha katika Suuratu Nnuur:30-31


قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ - 24:30
Wambie waumini wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa) na wazilinde tupu zao hili ni takaso kwao; bila ya shaka Allaah anazo habari za wanayoyafanya

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا-24:31
Na wambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika
28 views0 comments

Recent Posts

See All

BAADHI YA DUAA NA ADHKAAR MUHIMU

KUNUIA HAJJ NA UMRA Labbayka Allahumma Umra Nimekuitikia Ewe Mola, (nimenuilia) Umra Labbayka Allahumma Hajj Nimekuitikia Ewe Mola, (nimenuilia) Hajj TALBIYAH Labbayka-Llaahumma labbayk labbayka laa s

Yenye Kuhatarisha Nyumba za Waislamu - 2

Ummu Nasra Kuna mambo mengi ya wazi kabisa ambayo sheria yameyakataza katika Uislamu na jamii imeghafilika nayo.  Mambo hayo huchangia  kuharibika na kuhatarisha mfumo  mzima wa kiislam ndani ya majum

Yenye Kuhatarisha Nyumba za Waislamu -1

Ummu Nasra UTANGULIZI Hakika shukrani zote ni zake Allaah Subhaanahu Wata’ala, tunaemshukuru, tunaemtegemea, kumtaka msamaha na kutubu kwake. Tunajikinga Kwake Allaah Subhaanahu Wata’ala kutokana na

Al-Iman Society of Northamptonshire

Society of Northamptonshire, Based in Northampton Mosque and Islamic Centre, 72 Clare St, NN1 3JA

Email: info@al-iman.co.uk

Phone: 07961 284919

Registered Charity: 1117020

Copyrights
Quick Links

© 2018 by Al-Iman - All materials are Copyrights to Al-iman  |  Terms of Use  |   Privacy Policy